Friday, 18 October 2013







 ZITO BADO HAVIELEWI VYAMA




MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto, ameendelea kusisitiza kuwa hadi sasa hakuna chama chochote cha siasa kilichowasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu zake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kuvitaka vyama hivyo kuacha propaganda na kulichukulia suala hilo kisiasa.

Amesema hazungumzi suala hilo kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, bali anasimamia Sheria na kama hawataki, wamshauri Spika wa Bunge, Anne Makinda, avunje kamati yake.
“Napenda niwaambie nazungumzia suala hili si kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema bali Mwenyekiti wa PAC na ninasimamia sheria,” alisema.
Akizungumza jana katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, Zitto alisema tangu atoe tamko la kutaka vyama hivyo vijiandae kujieleza kwanini havijawasilisha ripoti hizo za ukaguzi, amekuwa akisikia kelele tu na hakuna chama chochote kilichotekeleza kisheria jukumu hilo la kuwasilisha taarifa zake kwa Msajili tangu 2009 kama vinavyodai.                            “Najua kuna vyama vinajitetea kuwa tayari vimefanya ukaguzi wa hesabu zake, sasa kama kweli ziko wapi hizo ripoti, Sheria iko wazi, ukaguzi ukikamilika ripoti inatakiwa kuwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), na Msajili na si kuzifungia kabatini,” alisisitiza Zitto.</p>
Alisema amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuwaandikia barua ya kisheria viongozi wa vyama tisa vinavyopata ruzuku ya Serikali, ya kuwaita mbele ya kamati hiyo, Oktoba 25, mwaka huu ili kujieleza kwanini hawajawasilisha ripoti hizo kwa Msajili kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Vyama hivyo ambayo vimeshakula Sh bilioni 67.7 bila kutoa ripoti ya matumizi yake ni CCM Sh bilioni 50.9, Chadema Sh bilioni 9.2, CUF bilioni 6.3, NCCR-Mageuzi Sh milioni 677, TLP Sh milioni 217, UDP Sh milioni 333, DP Sh milioni 3.3, APPT-Maendeleo Sh milioni 11 na Chausta Sh milioni 2.4.
Uchafu
“Ninajua vyama vyenye kelele ni hivi vikubwa vya CCM na Chadema, ambavyo ndio vilitakiwa kuwa mfano lakini ukweli uko wazi, hatuwezi kuwa mabingwa wa kusimama bungeni kushughulikia Serikali kwa matumizi mabaya wakati sisi wenyewe si wasafi,” alisema Zitto.
Alisema Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2009 iko wazi kuwa ni wajibu wa CAG kukagua hesabu za vyama vya siasa na kuwasilisha ripoti yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye naye anatakiwa atoe ripoti hizo kwenye gazeti la Serikali kila mwaka.
Alifafanua kwamba vyama hivyo vilitakiwa kuteua kampuni ya kufanya ukaguzi lakini kati yao, ni CCM na TLP tu vilivyoteua kampuni za kufanya ukaguzi huo na kupeleka kwa CAG kwa ajili ya uthibitisho, ingawa hata baada ya kuteua kampuni hizo, havikupeleka ripoti kama vilivyopaswa kufanya kisheria.
“Kwa miaka minne mfululizo, hakuna taarifa yoyote iliyomfikia CAG ya ukaguzi wa chama wala kutolewa kwenye gazeti la Serikali, na kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 14 (4), Msajili anatakiwa azuie ruzuku kwa chama ambacho kitashindwa kuwasilisha taarifa zake za ukaguzi, hili halijafanyika jamani kwa miaka minne sasa,” alisisitiza.
Alisisitiza kwa vyama hivyo, kuacha kuleta masuala ya ujanja na kuingiza siasa katika eneo linalohusu fedha za umma. “Nasisitiza mimi hapa sifanyi siasa natekeleza sheria, kama ni siasa tukutane kwenye majukwaa, naomba hawa wenzangu waache kubwabwaja huko nje…tuache kuingiza ujanjaujanja linapokuja suala linalohusu fedha za umma, nitaendelea kutetea fedha za umma hata nikinyongwa sijali,” aliapa.
Alionya kuwa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka, Bunge inaruhusu Kamati kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayeonesha dharau ikiwemo kifungo, hivyo endapo vyama hivyo vitashindwa kuwasilisha ripoti hizo kuna uwezekano wa kuadhibiwa ikiwepo kufungwa.
“Sheria hii inatoa mamlaka kwa kamati kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafunga hadi siku saba, namaanisha wakiendelea kubwabwaja wataenda Segerea hadi Ukonga, hapa natekeleza Sheria na si siasa,” alionya.
Kuhusu madai kuwa vyama hivyo havikuwa na fedha za kukagua mahesabu yao, wakati kazi ya ukaguzi ni ya CAG aliyesema hakuwa na fedha za kufanya hivyo, Zitto alisema kauli hiyo ni hizo hizo propaganda, kwa kuwa haiwezekani taasisi yenye mapato madogo kama Bodi ya Tumbaku, haina fedha kama ilizonazo CUF, lakini inafedha za kufanya ukaguzi, CUF isiwenazo.
Umaarufu


Akizungumza kwa hasira baadhi ya majina aliyopewa baada ya kuagiza vyama hivyo vizuiwe kupata ruzuku, alisema wamemuita majina mengi mabaya ikiwemo kudaiwa kuwa anatafuta umaarufu.
“Suala la umaarufu silihitaji kwa kuwa tayari nimeshakuwa maarufu, hao wanaosema, nina uhakika kabisa hakuna aliye maarufu kama mimi,” alisema.
Aliwataka kama kuna anayemzidi umaarufu kati ya waliozungumza kutetea vyama vyao, ajitokeze waende pamoja shule yeyote ya msingi, ili wanafunzi waulizwe nani kati yao na yeye wanayemtambua.
Kwa mujibu wa Zitto, ameamua kulivalia njuga suala hilo kwa kuwa inavyoonekana Msajili na CAG, wanaogopa vyama hivyo kwani taarifa ya mwisho kuwasilishwa kwa Msajili kuhusu ukaguzi ni ya CCM ya mwaka 2008, na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa mujibu wa Sheria.
Alisema Msajili alipaswa kuzuia ruzuku ya vyama hivyo miaka mitatu iliyopita, na kusisitiza kuwa yeye haogopi mtu ilimradi anasimamia Sheria.
Pamoja na hayo, kwa taarifa ambazo gazeti hili imezipata, Mutungi, jana alikutana na viongozi wa vyama vya siasa kujadili suala hilo, ingawa taarifa ya kilichojadiliwa haikuweza kupatikana.
Madai ya vyama Wakati Zitto akitoa kauli hiyo, Chadema jana iliitisha mkutano wa waandishi wa habari kudai kuwa madai ya PAC sio sahihi na hayana ukweli.
Katibu wa Baraza la Wadhamini ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha wa Chadema, Antony Komu alisema taarifa za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012 ilishakabidhiwa huku akionesha barua aliyodai ni ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye kumbukumbu CDA.112/123/01a/37 ya Septemba 4 mwaka 2012 kama uthibitisho.
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Jumapili iliyopita alisema chama hicho kiko tayari kwenda mbele ya PAC na hesabu zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje, Shirika la Ukaguzi la Taifa (TAC).
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema mahesabu yao yako safi, ila wameshindwa kukaguliwa kwa kuwa Serikali haijatoa fedha za kufanya ukaguzi.
Katibu Mkuu wa NCCRMageuzi, Samuel Ruhuza, alisema chama hicho kiko tayari kuwasilisha hesabu zake, ila walishindwa kuwasilisha baada ya kuelezwa kuwa CAG, ndiye aliyepaswa kukagua.

No comments:

Post a Comment