ZITO BADO HAVIELEWI VYAMA
MWENYEKITI wa Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto, ameendelea kusisitiza kuwa hadi sasa
hakuna chama chochote cha siasa kilichowasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu
zake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kuvitaka vyama hivyo kuacha propaganda na
kulichukulia suala hilo kisiasa.
Amesema hazungumzi suala
hilo kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, bali anasimamia Sheria na kama
hawataki, wamshauri Spika wa Bunge, Anne Makinda, avunje kamati yake.
“Napenda niwaambie
nazungumzia suala hili si kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema bali Mwenyekiti wa
PAC na ninasimamia sheria,” alisema.
Akizungumza jana katika
ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, Zitto alisema tangu atoe tamko la
kutaka vyama hivyo vijiandae kujieleza kwanini havijawasilisha ripoti hizo za
ukaguzi, amekuwa akisikia kelele tu na hakuna chama chochote kilichotekeleza
kisheria jukumu hilo la kuwasilisha taarifa zake kwa Msajili tangu 2009 kama
vinavyodai. “Najua kuna vyama vinajitetea
kuwa tayari vimefanya ukaguzi wa hesabu zake, sasa kama kweli ziko wapi hizo
ripoti, Sheria iko wazi, ukaguzi ukikamilika ripoti inatakiwa kuwasilishwa kwa
Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), na Msajili na si
kuzifungia kabatini,” alisisitiza Zitto.</p>
Alisema amemuagiza
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuwaandikia barua ya kisheria
viongozi wa vyama tisa vinavyopata ruzuku ya Serikali, ya kuwaita mbele ya
kamati hiyo, Oktoba 25, mwaka huu ili kujieleza kwanini hawajawasilisha ripoti
hizo kwa Msajili kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Vyama hivyo ambayo
vimeshakula Sh bilioni 67.7 bila kutoa ripoti ya matumizi yake ni CCM Sh
bilioni 50.9, Chadema Sh bilioni 9.2, CUF bilioni 6.3, NCCR-Mageuzi Sh milioni
677, TLP Sh milioni 217, UDP Sh milioni 333, DP Sh milioni 3.3, APPT-Maendeleo
Sh milioni 11 na Chausta Sh milioni 2.4.
Uchafu
“Ninajua vyama vyenye
kelele ni hivi vikubwa vya CCM na Chadema, ambavyo ndio vilitakiwa kuwa mfano
lakini ukweli uko wazi, hatuwezi kuwa mabingwa wa kusimama bungeni
kushughulikia Serikali kwa matumizi mabaya wakati sisi wenyewe si wasafi,”
alisema Zitto.
Alisema Sheria ya Vyama
vya Siasa ya 2009 iko wazi kuwa ni wajibu wa CAG kukagua hesabu za vyama vya siasa
na kuwasilisha ripoti yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye naye
anatakiwa atoe ripoti hizo kwenye gazeti la Serikali kila mwaka.
Alifafanua kwamba vyama
hivyo vilitakiwa kuteua kampuni ya kufanya ukaguzi lakini kati yao, ni CCM na
TLP tu vilivyoteua kampuni za kufanya ukaguzi huo na kupeleka kwa CAG kwa ajili
ya uthibitisho, ingawa hata baada ya kuteua kampuni hizo, havikupeleka ripoti
kama vilivyopaswa kufanya kisheria.
“Kwa miaka minne
mfululizo, hakuna taarifa yoyote iliyomfikia CAG ya ukaguzi wa chama wala
kutolewa kwenye gazeti la Serikali, na kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 14
(4), Msajili anatakiwa azuie ruzuku kwa chama ambacho kitashindwa kuwasilisha
taarifa zake za ukaguzi, hili halijafanyika jamani kwa miaka minne sasa,”
alisisitiza.
Alisisitiza kwa vyama
hivyo, kuacha kuleta masuala ya ujanja na kuingiza siasa katika eneo linalohusu
fedha za umma. “Nasisitiza mimi hapa sifanyi siasa natekeleza sheria, kama ni
siasa tukutane kwenye majukwaa, naomba hawa wenzangu waache kubwabwaja huko
nje…tuache kuingiza ujanjaujanja linapokuja suala linalohusu fedha za umma,
nitaendelea kutetea fedha za umma hata nikinyongwa sijali,” aliapa.
Alionya kuwa Sheria ya
Haki, Kinga na Madaraka, Bunge inaruhusu Kamati kuchukua hatua za kisheria
dhidi ya mtu yeyote atakayeonesha dharau ikiwemo kifungo, hivyo endapo vyama
hivyo vitashindwa kuwasilisha ripoti hizo kuna uwezekano wa kuadhibiwa ikiwepo
kufungwa.
“Sheria hii inatoa
mamlaka kwa kamati kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafunga hadi siku saba,
namaanisha wakiendelea kubwabwaja wataenda Segerea hadi Ukonga, hapa natekeleza
Sheria na si siasa,” alionya.
Kuhusu madai kuwa vyama
hivyo havikuwa na fedha za kukagua mahesabu yao, wakati kazi ya ukaguzi ni ya
CAG aliyesema hakuwa na fedha za kufanya hivyo, Zitto alisema kauli hiyo ni
hizo hizo propaganda, kwa kuwa haiwezekani taasisi yenye mapato madogo kama
Bodi ya Tumbaku, haina fedha kama ilizonazo CUF, lakini inafedha za kufanya
ukaguzi, CUF isiwenazo.
Umaarufu
Akizungumza kwa hasira
baadhi ya majina aliyopewa baada ya kuagiza vyama hivyo vizuiwe kupata ruzuku,
alisema wamemuita majina mengi mabaya ikiwemo kudaiwa kuwa anatafuta umaarufu.
“Suala la umaarufu
silihitaji kwa kuwa tayari nimeshakuwa maarufu, hao wanaosema, nina uhakika
kabisa hakuna aliye maarufu kama mimi,” alisema.
Aliwataka kama kuna
anayemzidi umaarufu kati ya waliozungumza kutetea vyama vyao, ajitokeze waende
pamoja shule yeyote ya msingi, ili wanafunzi waulizwe nani kati yao na yeye
wanayemtambua.
Kwa mujibu wa Zitto,
ameamua kulivalia njuga suala hilo kwa kuwa inavyoonekana Msajili na CAG,
wanaogopa vyama hivyo kwani taarifa ya mwisho kuwasilishwa kwa Msajili kuhusu
ukaguzi ni ya CCM ya mwaka 2008, na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa mujibu
wa Sheria.
Alisema Msajili alipaswa
kuzuia ruzuku ya vyama hivyo miaka mitatu iliyopita, na kusisitiza kuwa yeye
haogopi mtu ilimradi anasimamia Sheria.
Pamoja na hayo, kwa
taarifa ambazo gazeti hili imezipata, Mutungi, jana alikutana na viongozi wa
vyama vya siasa kujadili suala hilo, ingawa taarifa ya kilichojadiliwa
haikuweza kupatikana.
Madai ya vyama Wakati
Zitto akitoa kauli hiyo, Chadema jana iliitisha mkutano wa waandishi wa habari
kudai kuwa madai ya PAC sio sahihi na hayana ukweli.
Katibu wa Baraza la
Wadhamini ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha wa Chadema, Antony Komu alisema taarifa
za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012 ilishakabidhiwa huku
akionesha barua aliyodai ni ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye kumbukumbu
CDA.112/123/01a/37 ya Septemba 4 mwaka 2012 kama uthibitisho.
Naye Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Jumapili
iliyopita alisema chama hicho kiko tayari kwenda mbele ya PAC na hesabu
zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje, Shirika la Ukaguzi la Taifa (TAC).
Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema mahesabu yao yako safi, ila wameshindwa
kukaguliwa kwa kuwa Serikali haijatoa fedha za kufanya ukaguzi.
Katibu Mkuu wa
NCCRMageuzi, Samuel Ruhuza, alisema chama hicho kiko tayari kuwasilisha hesabu
zake, ila walishindwa kuwasilisha baada ya kuelezwa kuwa CAG, ndiye aliyepaswa
kukagua.